
Dar es Salaam.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya ametangaza rasmi nia ya
kugombea ubunge katika Jimbo la Bunda ambalo linashikiliwa na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira.
Kwa nia hiyo, Bulaya anaweza kuwa ametangaza vita
dhidi ya Wasira ambaye hivi karibuni akiwa Bunda, alitangaza kukitetea
kiti chake hicho katika Uchaguzi Mkuu 2015.
Julai 8, mwaka huu Wasira akiwa kwenye kikao cha
kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM wilayani Bunda, alitangaza kuwa
atatetea nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu ujao, huku akijigamba kuwa
yeye ni “mwarobaini wa matatizo” yanayowakabili wakazi wa jimbo hilo.
Kabla ya kutangaza nia hiyo, mara kadhaa Wasira
amekuwa akihusishwa na suala la urais na ni mmoja wa makada sita wa CCM
ambao walipewa adhabu na chama hicho Februari 18 mwaka huu, baada ya
kukutwa na makosa ya kuanza mapema kampeni za urais mwaka 2015.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti
hili jana, Bulaya alisema atagombea ubunge katika Jimbo la Bunda na
anamtakia kila heri mpinzani wake huyo (Wasira) katika nafasi ya juu ya
urais anayotaka kuwania. Alisema ameamua kufanya hivyo baada ya kuombwa
na watu kadhaa kutoka jimboni humo wakiwamo vijana, wazee na kinamama.
“Ninaamini nimepata uzoefu mkubwa katika kipindi
hiki cha ubunge wa viti maalumu na ninawataka wabunge wenzangu wa viti
maalumu waone kuwa nafasi hiyo ni fursa ya kujifunza, lakini mwisho wa
yote lazima urudi jimboni,” alisema.
“Hii ni mara ya kwanza nasema hapa. Nitagombea
ubunge Jimbo la Bunda kwa kuwa nimeombwa sana na vijana, wazee na ni
mara nyingi nimekuwa nikisema bado muda, lakini sasa umebaki muda mfupi
hivyo niseme tu kwamba nitagombea. Uongozi ni mbio za kupokezana vijiti.
Wasira ni kama baba yangu na sina ugomvi naye na namtakia kila la heri
katika position (nafasi) yake nyingine anayoitaka,” alisema.
Kuhusu madai kwamba Wasira anafikiria kuwania
urais, alisema, “Naona ni uamuzi sahihi amefanya, kwani amekuwa mbunge
tangu mimi nazaliwa mwaka 1980 ameona kwamba ni kweli hii position
(nafasi) ya chini ameshaitumikia sana, hivyo ameona katika uzoefu
alionao labda ajaribu katika nafasi ya urais.”
Bulaya alisema si kwamba ameamua kugombea ubunge
wa Bunda kwa kuwa Wasira anataka urais, bali viti maalumu alipo hivi
sasa ni njia ya kupata uzoefu na kujifunza katika kuelekea kugombea
ubunge wa jimbo.
“Ili kuondoa suala la kwamba viti maalumu ni vya
kupewa siyo kwamba nasema vifutwe, lakini unaweza ukawekwa utaratibu
mwingine wa kumpa mwanamke uzoefu katika ngazi ya kibunge,” alisema na
kuongeza;
“Lakini unapopewa hebu itendee haki hiyo fursa,
kama mtu umeingia viti maalumu unajifunza na unakwenda kugombea na huko
kuna kushinda na kushindwa lakini ni lazima nionyeshe hii fursa nimepewa
naweza kwenda kushindana na wanaume.”
Alisema hilo ni jambo la msingi kwa kuwa huwezi
kulemaa kwa kuwa mbunge wa viti maalumu bila kujifunza na kukaa miaka
hadi 15 kwenye ubunge wa aina hiyohiyo kwani wako wengine wanaotakiwa
kupata nafasi hiyo ili wajifunze na kwenda majimboni.
0 comments:
Post a Comment