
Na Baraka Mpenja
WAGONGA nyundo wa Mbeya, Mbeya
City fc wametandikwa mabao 4-1 na Vipers FC (Zamani Bunamwaya)
inayoshiriki ligi ya Uganda katika mechi ya kimataifa ya kirafiki
iliyomalizika jioni ya leo uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Vipers FC waliowasili leo asubuhi jijini humo walitandaza soka safi na kuwazidi wenyeji wao karibia idara zote.
Hata hivyo taarifa kutoka kwa
shuhuda wetu aliyekuwepo uwanjani hapo, Mbeya City walijitahidi
kugangamala, lakini walionekana kutokuwa na ushindani wa ngazi ya
kimataifa.
Mechi hiyo ni ya mwisho ya
kujipima ubavu kwa kocha Juma Mwambusi ambaye ana changamoto ya kufanya
vizuri katika msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara unaotarajia kuanza
kutimua vumbi septemba 20 mwaka huu.
Mwambusi aliyeibuka kuwa kocha
bora msimu uliopita, anasaidiwa na Suleiman Jabiri baada ya msaidizi
wake Maka Mwalwisyi kukataa kuongeza mkataba muda mfupi baada ya ligi
kuu msimu uliopita kumalizika.
Maka kwasasa ni kocha mkuu wa klabu ya Panone FC ya mkoani Kilimanjaro na inashiriki ligi daraja la kwanza.
Mbeya City msimu uliopita walimaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na mabingwa Azam fc.
Wakali hao wanaovalia jezi za
zambarao wataanza kampeni ya ligi kuu msimu wa 2014/2015 kwa
kuwakaribisha JKT Ruvu katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, septemba
20 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment