
Mwenyekiti
wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akipiga kura wakati wa Mkutano Mkuu wa
chama hicho huku akiwa jirani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Picha ya
Maktaba
Dodoma.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameingia rasmi katika mbio za kuwania urais
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), hatua ambayo imebadili mwelekeo wa
kinyang’anyiro cha nafasi hiyo kubwa ya uongozi nchini kuelekea Uchaguzi
Mkuu 2015.
Gazeti
hili limethibitisha kwamba Pinda tayari ameamua kujitosa kuwania nafasi
hiyo kupitia CCM ambayo tayari inawaniwa na makada wa chama hicho
wasiopungua 15 na baadhi yao wameishatangaza nia zao kwa nyakati
tofauti.
Habari
kutoka ndani ya CCM zinasema uamuzi wa Pinda kuwania urais mwaka mmoja
tu kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwakani,
umesababisha kiwewe miongoni mwa wagombea na kunakifanya kinyang’anyiro
hicho kuchukua sura mpya.
Kiongozi
mmoja mwandamizi wa CCM aliliambia gazeti hili siku chache zilizopita
mjini Dodoma kuwa: “Na sisi tumesikia kwamba PM (Waziri Mkuu) amejitosa
na kama ni kweli atawasumbua wagombea wengi kutokana na rekodi yake hasa
katika uadilifu.”
“Yeye
(Pinda) ana faida tatu kubwa; kwanza hana kundi katika chama, anaelewana
na watu wote, pili nafasi yake ya uwaziri mkuu inampa nafasi ya
kufahamika kwa watu wengi na tatu rekodi yake ya uadilifu, hana kashfa
za ovyoovyo, labda kama ataharibu dakika hizi za mwisho,” alisema
kiongozi huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Wengine
ambao wamekuwa wakitajwa kuwania uraia kupitia CCM ni Waziri Mkuu wa
zamani Edward Lowassa na mtangulizi wake katika nafasi hiyo, Frederick
Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark
Mwandosya, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wegine ni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Bunge Maalumu, Samuel Sitta. Wengine wanaotajwa ni Waziri wa Uchukuzi,
Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Katiba, Asha-Rose Migiro.
Pia wamo
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Naibu Waziri wa
Fedha, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mbunge wa
Msalala, Ezekiel Maige na aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini
Ujerumani, Balozi Ali Karume.
Wasomi
Profesa
wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho alisema wingi wa
wanaojitokeza kutaka kuwania urais ni njia ya kuunda mtandao
utakaomwezesha mtu fulani au mmoja kunyakua tiketi hiyo.
“Watu
wanapiga kampeni katika harambee kwa njia ya kutengeneza mitandao, kwani
ukifika wakati wa chama kumpitisha mgombea, asiposhinda ataibuka na
kuwaeleza kuwa mnaoniunga mkono mimi muungeni fulani,” alisema.
Naye
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema
kujitokeza kwa idadi kubwa ya wanaowania nafasi ya urais, kutatoa fursa
ya wananchi kutambua udhaifu wa kila mmoja jambo litakalowezesha
kupatikana kwa mtu sahihi wa kupeperusha bendera ya chama hicho.
“Wakiwa
wengi, kila mmoja atataka kuonyesha umahiri wake na sisi ambao ni
wananchi watawaliwa tutaweza kutambua upungufu wa kila mmoja, jambo
litakalosaidia kupatikana kwa mtu sahihi,” alisema Mbunda
Kambi ya Pinda
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili kwa siku kadhaa mjini Dodoma ambako vikao vya
Bunge Maalumu vinaendelea umebaini kuwa kambi ya Pinda inaongozwa na
Mwenyekiti wa Mamlaka za Mitaa Tanzania (ALAT) ambaye pia ni Meya wa
Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi.
Inadhaniwa
kuwa Dk Masaburi atatumia ushawishi wake kwa viongozi wa mamlaka za
miji na wilaya zinazoongozwa na wenyeviti wa halmashauri na mameya wa
miji, manispaa na majiji kumuunga mkono mgombea huyo ambaye pia hivi
sasa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ziko chini ya ofisi yake.
Wiki hii
kundi la wafuasi wa Pinda likiongozwa na Dk Masaburi lilikuwa mjini
Dodoma likijaribu kutafuta kuungwa mkono na makada viongozi wa CCM ambao
walikuwa wakishiriki kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho pamoja na wale
walioko katika Bunge Maalumu. Habari zinasema mbali na Dodoma, tayari
kambi hiyo imeshafanya vikao kadhaa jijini Dar es Salaam na Visiwani
Zanzibar lengo likiwa ni kutafuta kuungwa mkono na makada wa CCM katika
sehemu hizo. Hivi sasa nguvu za Pinda zinaelekezwa katika mikoa mingine
nchini kwa lengo hilohilo. Kutokana na kasi ya kambi yake, wafuasi wa
baadhi ya wagombea wameanza kufuatilia mwenendo wao kwa lengo la
kukusanya ushahidi wa kile wanachokiita ‘rafu’ zinazochezwa ili kupata
ushahidi unaoweza kutumika dhidi ya mgombea huyo wakati mchakato wa
uchaguzi ndani ya CCM utakapoanza mapema mwakani.
Itakumbukwa
kwamba makada watano wa chama hicho ambao ni Lowassa, Membe, Makamba,
Wassira na Ngeleja wanatumikia adhabu na wapo chini ya uangalizi wa
chama hicho baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kuanza kampeni za
urais kabla ya muda kutangazwa.
Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema hivi sasa ni mapema mno kusema
ni lini mchakato wa kupata wagombea wa nafasi za uongozi ndani ya chama
hicho utaanza na kwamba wakati mwafaka ukiwadia wananchi watafahamishwa.
Uwezo, udhaifu wake
Hata
hivyo wakosoaji wake wanasema Pinda akiwa Waziri Mkuu hana cha kujivunia
na kwamba amekuwa mzito kufanya uamuzi mara kadhaa kiasi cha
kusababisha baadhi ya mambo muhimu ya nchi kukwama na kwamba kwa maana
hiyo hastahili kuwa rais.
“Ni kitu
gani ambacho nchi inakikumbuka kuhusu huyu bwana ambacho alikifanya
katika miaka yake ya uwaziri mkuu, kama alikuwa kwenye nafasi kubwa
kiasi hicho na hakuna alichofanya, atawezaje kumudu madaraka ya mkuu wa
nchi?” alihoji mmoja wa makada wakongwe wa CCM.
Waziri
mmoja wa sasa (jina tumelihifadhi), alisema Pinda hana uwezo wa kuongoza
nchi, kwani wao wakiwa mawaziri ameshindwa kuwasaidia katika kero
mbalimbali walizokuwa wakimfikishia kama kiongozi wao.
“Muulize
waziri yeyote kuhusu uwezo wa jamaa, kila kukicha tunampelekea mambo
tunayokutana nayo, lakini hakuna kinachowezekana kwake, atakwambia
subiri leo, subiri kesho na hatimaye jambo linaishia hivyohivyo,”
alisema.
Kwa
upande mwingine, watetezi wake wanasema Pinda wanayemnadi ni yule
aliyepata kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa – Tamisemi) kiasi cha kuonekana anafaa kuwa Waziri
Mkuu.
Wanasema
kushindwa kwake kufanya kazi ipasavyo ni matokeo ya sababu zilizomfanya
mtangulizi wake, Lowassa kung’oka katika nafasi yake.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment