
Na Hebel Chidawali
Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, kutoka Kundi la 201, Thomas Mgoli
amelazwa katika Hospitali ya Dodoma baada ya kupigwa na watu aliodai
kuwa ni wafuasi wa Chadema.
Mjumbe huyo alidai kuwa kati ya watu waliompiga yumo mtumishi wa Bunge
na ameshamshtaki kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta huku
akisema akimuona anaweza kumtambua.
Mgoli ambaye anatokea Chama cha Alliance Democratic Change (ADC),
alisema kuwa alipokea kipigo kikubwa juzi katika maeneo ya Area A karibu
na Shule ya Msingi Chamwino A.
Akiwa katika wodi ya daraja la kwanza hospitalini hapo, alieleza kuwa
chanzo cha mapigano hayo ni mabishano waliyokuwa nayo na vijana wanne
mmoja aliyemtaja kwa jina la Vampaya.
“Nimepanga nyumba katika eneo hilo, juzi (jana) saa mbili usiku nilitoka
kwenda grocery (duka la vinywaji) kuchukua kinywaji ili nirudi
nyumbani. Niliwakuta vijana hao ambao wakati wote tumekuwa tukitaniana,”
alisema na kuongeza:
“Mara baada ya kufika wakaniuliza katika mchango wangu bungeni ni kwa
nini nilimtukana Profesa Kabudi (Palamagamba), nikajaribu kueleza
kilichotokea bungeni na kuhusu mchango wangu, basi wakaanza kunipiga
ngumi nilipotaka kukimbia nikapigwa na kipande cha tofali.”
Mjumbe huyo alidai kuwa ni kawaida kukutana na vijana hao katika duka hilo na kupata vinywaji huku wakitaniana.
Sitta alifika hospitalini hapo kumjulia hali na alielezwa mkasa mzima.
Baadaye Sitta aliwaonya wajumbe wa Bunge lake kuwa mijadala ya Katiba
inapaswa kufanyika ndani ya Bunge na siyo nje huku akiwasihi Watanzania
kuwa wavumilivu ili Katiba bora ipatikane.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Mzee Nasoro alisema hali ya
mgonjwa huyo inaendelea vizuri na kwamba alikuwa na maumivu ya juu
katika maeneo ya usoni na mdomoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema tukio lilitokea
wakati mjumbe huyo alipokuwa akipata kinywaji katika duka hilo ndipo
kukatokea mabishano yaliyosababisha kupigwa kwake.
Alisema polisi wanaendelea kuwahoji watu watatu ili kupata ukweli wa jambo hilo.
Kutoka: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment